• Breaking News

    USHAURI, ELIMU na TIBA YA ASILI +255 767-759-137

    Monday, 1 May 2017

    Kumbe Unaweza Kupunguza Uzito Wako Kuanzia Leo



    Uzito mkubwa ni nini?

    Kulingana na viwango vya kimataifa vya shirika la afya la dunia (WHO) vilivyotokana na  tafiti mbalimbali uzito wa mtu unapimwa kwa mfumo wa BMI ( Body mass index).
    BMI inapatikana kwa kugawanya uzito katika kg kwa kipeo cha 2 cha urefu katika mita.
    Kwahiyo,
    BMI=Uzito (kg)/urefu^2 (m^2)

    Baada ya kufahamu huu mfumo wa kupima uzito wa mtu. Uzito sasa umegawanywa katika makundi mbalimbali kama ifutavyo
    • chini ya 18.5 ni uzito mdogo kupita kiasi (underweight)
    • 18.5-25 ni uzito sawa (normal weight)
    • 25-30 ni uzito mkubwa kupita kiasi (overweight)
    • 30+ ni kiriba tumbo (obesity)

    Kwa hiyo baada ya kupata hesabu ya BMI unaweza kuangalia unaangukia kwenye kundi gani hapo juu.

     Sababu zinazopelekea kuongezeka uzito kupita kiasi

    1. VYAKULA NA VINYWAJI VYA SUKARI
    Vyakula kama keki na vinywaji kama soda na jamii zake ( vyenye sukari nyingi) hupunguza uwezo wa seli kuhisi insulini.

    Ikumbukwe kuwa seli zote za mwili isipokuwa za ubongo huhitaji insulini ili kuchukia sukari kutoka kwenye damu. Kwa hiyo unapopunguza uwezo wa seli kuhisi insulini unaongeza kiwango cha sukari kwenye damu ambayo mwili ( ini) utaibadilisha na kuwa fati ambayo itaongeza uzito wako pamoja na kitambi.

    2. POMBE
    Unywaji wa pombe sana husababisha kuzuia uunguzwaji wa fati iliyolundikana mwilini kuwa sukari ili itumike kutengeneza nguvu matokeo yake ni kuongezeka uzito.

    3. Mafuta ambayo yanatokana na wanyama au mafuta ambayo yamekaangwa sana.

    Tafiti zinaonesha kuwa mafuta haya yanaweza kuleta madhara. Yanaweza kusababisha kuongeza ukinzani wa seli kuhisi insulini na hata matatizo ya moyo.

    [VIDEO] Vyakula vya mafuta mengi na athari zake

    4. KUTOJISHUGHULISHA MWILI
    Hii inapelekea mwili kulimbikiza chakula hicho tumboni na sehemu zingine hivyo kusababisha kuongezeka kwa uzito

    5. PROTINI KIDOGO KATIKA MLO
    Chakula chenye protini husaidia mtu kujisikia kashiba na kuepusha kula sana kupita kiasi.
    Kama protini kwenye mlo wako ni kidogo, kimeng'enya kinachoitwa NPY kinazalishwa kuleta hamu ya kula. Hivyo unakula na kusababisha kuongezeka chakula kisicho na matumizi mwilini na hivyo kuongezeka uzito hatari.

    6. MENOPOZI
    Hiki ni kipindi ambacho mama anafikia na anakoma kupata siku zake ( kwa sababu ya umri) hapa hakuna kichocheo kinachoitwa estrojeni.

    Estrojen ni kichocheo ambacho kinasaidia kuelekeza fati kukaa kwenye mapaja pamoja na makalio ya mwanamke kwa namna nzuri kwa afya. Kama kichocheo hiki hakipo mwili fati inayoongezeka inapelekwa kwenye maeneo mengine hasa tumbo. Hivyo kusababisha kuongezeka uzito au kitambi.

    7. MSONGO WA MAWAZO
    Msongo wa mawazo kusababisha kuzalishwa kwa kichocheo kinachoitwa cortisol ambacho kinaunguza chakula mwilini na kusababisha  mtu kula sana.
    Badala ya fati inayoongezeka kutunzwa sehemu zote za mwili cortisol husabisha fati ihifadhiwe eneo la tumbo.

    8. MLO WENYE VYAKULA VYA NYUZI NYUZI CHACHE
    Vyakula vyenye vyuzi vyuzi husaidia kujisikia hisia ya kutosheka na kuepusha kula sana.

    9. VINASABA
    Shughuli zote za mwili zinatawaliwa na vinasaba ( DNA) hivyo hata suala la kubadili sukari kuwa fati au kinyume chake zinatawaliwa na hivi vinasaba.

    10. KUKOSA USINGIZI
    Tafiti zinaonesha watu ambao hawapati usingizi wa kutosha kila siku au ambao wanapata usingizi wenye ubora kidogo/ hafifu wanakabiliwa na shida ya kuongezeka uzito pamoja na kitambi.
    Kitambi ni hatari hata kama una uzito wa kawaida kiafya. Athari za kitambi ni sawa na zile za mtu mwenye uzito mkubwa. Kama vile magonjwa ya moyo na kisukari.

    Sababu zote hizi zinaathiri watu kwa namna mbalimbali na hivyo hata namna ya kupambana nayo njia zinatofautiana.

    Lakini yote katika yote usikubali kuwa na kitambi au uzito mkubwa sana ni HATARI kwa afya na maisha yako kwa ujumla.

    ATHARI ZA UZITO MKUBWA

    Mwingine anaweza akaona ni fahari kuwa na uzito mkubwa kuliko kawaida au kuwa na kitambi. Hata hivyo wapi  ambao wanaona kitambi kama ufahari kama kiashirio cha kuwa na Mali. Hata hivyo kiafya ni hatari.
    Uzito mkubwa kupita kiasi unaambatana na bando la magonjwa makubwa ambayo ni hatari kwa maisha ya mtu.

    Magonjwa hayo ni haya:

    1.MAGONJWA YA MOYO NA MFUMO WA DAMU
    Uzito mkubwa kusababisha magonjwa ya mishipa ya damu ya moyo ( coronary vessels) na hivyo inaweza kuathiri utendaji kazi wa moyo.
    Na hata mishipa ya damu ya sehemu zingine za mwili inaweza kuathiriwa na mafuta ambayo yamejazana mwilini na kusababisha athari mbambali.

    Mfano:
    - mishipa ya damu ya ubongo itakapo athiriwa sehemu ya ubongo haitapata damu na mtu atapata kiharusi ( kulemaa sehemu ya mwili au mwili wote)
    -  pia kusinyaa kwa mishipa ya damu kunaongeza shinikizo la damu na hivyo kusababisha matatizo mengine katika ini na figo.

    2. KISUKARI AINA YA 2
    Watu wenye kisukari aina ya 2 wengi kinatokana na uzito kuwa mkubwa sana au kitambi.
    Hata hivyo hasara za kisukari katika mwili ziko wazi. Hivyo kwa kuruhusu kitu kimoja mlolongo wa matatizo hufunguliwa mlango.

    3. OSTEOARTHRITIS
    Huu ni ugonjwa ambao unahusisha kulika au kuvunjika kwa gegedu na mifupa katika eneo la viunganishi (joint).
    Hii kusababisha maumivu na mtu kushindwa kutembea vizuri au kukosa Uhuru wa kufanya vitu hasa kuhusisha joint za mifupa yake.

    4. SARATANI
    Tafiti zinaonesha kuwa UZITO mkubwa na kitambi vinahusika na saratani zifuatazo; ukuta wa ndani wa mji wa mimba (endometrium), matiti, utumbo mkubwa, figo, mfuko wa nyingi ( gallbladder) na ini.

    5. MATATIZO YA KUPUMUA ( sleep apnea)
    Hii shida ambayo inatokea mtu anapokuwa amelala. Kunakuwa na vipindi ambavyo anaacha kupumua lakini pia pumu (asthma) inaweza kujitokeza.

    6. GOUT
    Huu ni ugonjwa ambao unatokana na mlundikano wa uric asidi nyingi kwenye damu. Inapokuwa nyingi Mara nyingi hukaa kwenye jointi za mwili na hapo kuleta shida katika maeneo hayo.

    7. KUSHUKA KWA UBORA WA MAISHA
    Ni kweli kwamba kuwa na uzito mkubwa sana na kitambi unakosa Uhuru wa kufanya mambo mengi kwa Uhuru.
    Na wakati mwingine unaweza kuonekana kama mgonjwa. Hata hivyo hatari ya magonjwa yanayokunyemelea hushusha ubora wa maisha ambayo ungekuwa nayo.

    8. HEMORRHOIDS/BAWASIRI
    Huu ni ugonjwa ambao mtu anaota kinyama katika sehemu ya haja kubwa na kusababisha maumivu, kuwasha au hali ya usumbufu. Hii hutokana na kutanuka kwa mishipa ya damu katika eneo hilo kutokana na damu kuzuiliwa kurudi kwenye moyo kupitia mishipa Fulani.

    Ikumbukwe kuwa magonjwa haya huathiri watu kwa namna tofauti kulingana na mifumo ya mwili na vinasaba vya mtu husika. Hata hivyo usijihatarishe kwa kuendekeza uzito mkubwa.

    NJIA ZA KUPUNGUZA UZITO MKUBWA

    Njia za kutatua zinatofautiana kutoka mtu hadi mtu kulingana na asili ya miili pamoja na mazingira mtu aliyopo.
    Hapa nitaeleza njia za jumla na mtu binafsi ataangalia kuona ni ipi hasa inamfaa kwa wakati huu.

    1. EPUKA VITU VINAVYOSABABISHA KUONGEZEKA UZITO AU KUPATA KITAMBI
    Rejea sababu zinazopelekea mtu kupata kitambi au kuongezeka uzito. Njia ya kwanza ni kuepukana na vyanzo hivyo. Hata hivyo baadhi yake nimevijadili hapa chini.

    2. TUMIA CHAKULA NA MTINDO WAKO WA MAISHA KUJITIBU
    Fanya yafuatayo kuondokana na shida hii.
    a) choose low carb diet (chagua vyakula vyenye kiwango kidogo cha sukari)
    Mfano: mkate, mboga za majani n.k

    Epuka vyakula vyenye sukari nyingi na kabohaidreti nyingi. Hii itasaidia mwili wako kutengeneza insulin kidogo na hivyo kuharakisha fati kuunguzwa na kupungua uzito.

    b) kula pale tu unapokuwa na njaa
    Ili kupunguza uzito inashauriwa kula pale tu unapokuwa na njaa. Epuka kula kula ovyo.

    c) kula vyakula halisi.
    Vyakula halisi ni vile ambavyo havijachakatwa kiwandani na kuongezewa vitu kama rangi ya chakula bandia na vikolezo bandia. Tumia vyakula kama; nyama, samaki, mbogamboga, mayai, karanga n.k

    d) Pima maendeleo yako kwa busara.
    Ni jambo la muhimu sana kujua maendeleo yako wakati unaendelea na zoezi la kupunguza uzito wako.
    Kanuni ya kujipima:
    1. weka tape measure katikati angalau huu ya kitovu na juu ya mfupa wa kiuno ( hipbone) pembeni.
    2. toa hewa nje na jilegeze
    3. usigandamize ngozi unapochukua vipimo
    Fanya hivyo unapoanza na unavyoendelea na zoezi. Kisha linganisha na vipimo vinavyokubalika kiafya.

    Wanaume:
    <94 cm - nzuri sana
    94-102 cm nzuri
    102> - mbaya

    Wanawake:
    <80cm nzuri sana
    80- 88cm nzuri
    88cm > mbaya

    e) usiache kufanya hivi.
    Wengi wamekuwa wakipata shida ya kujikuta wanarudi katika hali yao ya zamani kwa sababu baada ya kupunguza uzito wanabweteka na kusahau.

    Ikumbukwe kuwa suala la uzito ni la kila Siku. Wewe ambaye Leo uko sawa ukiwa na mtindo mbaya wa maisha utajikuta umo katika kundi hili. Hivyo wote tunapaswa kuchunga sana namna tunavyokula, na kufanya shughuli zetu za kila siku.

    f) epuka pombe
    Tafiti zinaonesha kuwa pombe huzuia vimeng'enya ambavyo huvunja fati ya mwili na hivyo kufanya iongezeke zaidi na zaidi hasa sehem ya tumbo.

    g) epuka msongo wa mawazo na lala Masaa ya kutosha.
    Msongo wa mawazo husababisha kuzalishwa kwa kichocheo ambacho husababisha mtu kula sana na hivyo kuongeza uzito.

    Punguza msongo wa mawazo kwa kadri inavyowezekana. Jaribu kufikiria vitu katika namna chanya na pia amini Mungu tafiti zimeonesha kuwa inasaidia.
    Pia hakikisha unapata usingizi wa kutosha kila Siku angalau masaa 6 kwa siku ya kusinzia. Itakusaidia sana.

    h) pata virutubisho vya vitamini na madini.
    Haya ni muhimu kwa ajili ya utendaji kazi wa mwili. Unapoyakosa mwili unaleta hamu ya kula hata kama chakula ni kingi mwilini ili angalau kupatikane vitamini na madini ya kutosha kwa ajili ya mwili. Hivyo pata virutubisho hivi vya kutosha. Hasa  vitamin D imeonekana kuwa saidia sana watu wenye uzito mkubwa.

    h) mifungo ya Mara kwa Mara.
    Kufunga kula sio mateso. Mara nyingi imekuwa ikihusianishwa na ibada. Lakini wanasayansi wamagundua kuwa ni tiba nzuri kwa wenye uzito mkubwa. Hata kwa wengine pia inamanufaa mengi kiafya ikiwemo kuondoa sumu mwilini.
    Funga Mara nyingi kadri uwezavyo itasaidia sana katika harakati zako za kupambana na uzito mkubwa.

    [VIDEO] Kufunga na Afya- Namna ya Kufunga ili upate matokeo mazuri


    I) Fanya mazoezi
    Huenda ungetegemea njia hii iwe ya kwanza katika orodha lakini nimeiweka karibu na mwisho kwa maana Mazoezi hayana cha kufanya kumsaidia mtu kupunguza uzito kama njia hizo juu hazifuatwi. Mazoezi huchangia 20% ya matokeo yako katika kupunguza uzito na 80% iliyobaki ipo katika chakula.

    Mfano; mtu atafanya mazoezi sawa lakini baada ya hapo anakula sana na hatimaye anaongeza kiasi kukubwa cha fati kuliko hata ile iliyovunjwa wakati wa mazoezi. Hata hivyo inachukua muda mrefu sana mtu kupunguza uzito ipasavyo kwa mazoezi pekee. Inaweza kukuchukua hata mwaka kufanikiwa. Hata hivyo mazoezi ni muhimu.  Fanya mazoezi angalau dakika 30 kila siku kwa siku 5 kwa wiki. Unaweza kufanya zaidi.

    Tunatamani kusikia kutoka kwako..... Andika comment yako hapa chini.


    Wako katika kuboresha afya, 
    (Dr Nature)



    Share kwa wengine, wasaidie wasisumbuliwe tena na shida hii.


    1 comment:

    1. Asante kwa ushauli mungu atulinde sote

      ReplyDelete